Rais William Ruto amesema uhusiano kati ya Kenya na Shirika la Umoja wa Mataifa ni thabiti na wenye urafiki mkubwa.
Alidokeza kuwa Umoja wa Mataifa umekuwa Mshirika Mkuu wa Kenya hasaa katika kawi safi, ufadhili, kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na kuwasaidia wakimbizi.
“Huku ikiwa mwanchama anayejivunia wa Umoja wa Mataifa, Kenya imetoa mchango mkubwa hasaa katika shughuli za kudumisha amani kote duniani, kuongoza wananchama katika miradi ya mabadiliko ya Tabianchi na mtetezi mkuu wa mageuzi katika Baraza la usalama,” alisema Rais Ruto.
Kiongozi huyo wa taifa aliongeza kuwa Kenya imekuwa na fahari ya kuwa mwenyeji wa Makao Makuu ya shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira UNEP, na lile kuhusu makao la UN-Habitat.
Aliyasema hayo leo Jumanne, kwenye hafla ya kumuaga Mshirikishi mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Kenya anayeondoka Stephen Jackson, katika Ikulu ya Nairobi.
Rais Ruto alimshukuru kwa huduma zake alizotoa akiwa hapa nchini, huku akimtakia heri njema katika shughuli zake za baadaye.