Rais Ruto: Uchumi wa Kenya umeimarika

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais William Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua.

Rais William Ruto amewahakikishia Wakenya kuwa uchumi umerudi sawa na nchi inatazamiwa kuwa na nyakati bora zaidi.

Rais alibainisha kuwa licha ya nyakati ngumu za kiuchumi, serikali iliendelea kuwa imara katika kufanya maamuzi sahihi kwa nchi, maamuzi aliyosema yamezaa matunda.

Alitaja kuimarika kwa hivi majuzi kwa shilingi ya Kenya dhidi ya dola na azimio la Eurobond ya dola bilioni mbili.

Kwa hiyo, bei ya bidhaa za vyakula kama vile unga wa mahindi na mafuta zimepungua kwa kiasi kikubwa, dalili za wazi za kuimarika kwa uchumi.

“Uchumi wetu ulikuwa mbaya na tulilemewa na madeni. Hata hivyo, ndani ya mwaka mmoja, tumerekebisha kila kitu,” alisema. “Huu ni mwaka ambao tutawasilisha ajenda ya maendeleo ya serikali. Kenya inaenda mahali.”

Rais aliwapongeza Wakenya kwa subira yao wakati nchi ilikuwa inapitia nyakati ngumu.

“Tutasongesha mbele nchi yetu kupitia umoja, kufanya kazi pamoja na kuchukua hatua za ujasiri zitakazoweka nchi yetu kwenye njia ya utulivu na ukuaji,” aliongeza.

Rais Ruto alisema hayo alipozindua ujenzi wa barabara ya Longisa-Sigor-Chebunyo na Kyogong-Sigor katika eneo bunge la Chepalungu, kaunti ya Bomet.

Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, Waziri wa Miundombinu Kipchumba Murkomen, Gavana wa Bomet Hillary Barchok, Viongozi wa Wengi Kimani Ichungwa (Bunge la Kitaifa) na Aaron Cheruiyot (Seneti), Wabunge na Wawakilishi wa Wadi kadhaa walihudhuria.

TAGGED:
Share This Article