Rais William Ruto amesema Serikali imejitolea kufanikisha utoaji wa Huduma za afya kwa wote.
Serikali, aliongeza, itaweka kipaumbele kwa huduma ya afya ya kinga, inayozingatia wafanyakazi wa afya ya jamii, mageuzi ya NHIF, na utoaji wa vifaa vya matibabu ili kuafikia lengo la kuhakikisha Afya Bora kwa Wote.
“Kumekuwa na majaribio mawili yaliyoshindwa kutekeleza huduma ya afya kwa wote. Lakini wakati huu, tumedhamiria kuifanikisha.
Huduma ya afya ya kinga itawezesha kushughulikia maswala ya afya mapema katika kiwango cha kijamii, jambo ambalo litapunguza msongamano hospitalini.”
Akizungumza alipokutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Hazina ya Global Fund Peter Sands katika Ikulu ya Nairobi, Rais Ruto alisema ni sharti Shirika la Ugavi wa Dawa nchini (KEMSA) kuboresha utoaji wake wa huduma.
“Kemsa ni sehemu muhimu ya mpango huu. Ni lazima watekeleze wajibu wao ipasavyo. Shirika hili limekuwa na matatizo, lakini tunayatatua,” alisema Rais.
Rais aidha alisema Serikali itaondoa ufisadi na walaghai katika NHIF ili kuifanya iwe na ufanisi zaidi.
Sands alisema Kenya ina “uhusiano mzuri” na Global Fund. Alimpongeza Rais Ruto kwa hatua madhubuti ya hivi majuzi ya kusafisha Kemsa.
Alisema Global Fund inaunga mkono ajenda ya Serikali ya huduma ya afya kwa wote na iko tayari kutoa utaalamu wa kiufundi.