Rais Ruto: Teknolojia na uvumbuzi zitaimarisha sekta ya usalama

Tom Mathinji
2 Min Read

Rais William Ruto amesema serikali inakumbatia mbinu mpya katika kudhibiti changamoto za kiusalama zinazochipuza.

Alidokeza kuwa serikali imejitolea kuimarisha elimu miongoni mwa maafisa wa usalama, ili kuwatayarisha kuhusiana  na changamoto za ulimwengu wa sasa.

Alisema hatua hiyo inalenga kuwapa maafisa wa usalama ujuzi na utaalam unaohitajika kukabiliana na changamoto za kiusalama.

“Kwa muda mrefu Sekta ya usalama na ulinzi zilionekana zisizokuwa na elimu pekee, mbali pia zisizotilia umuhimu mawazo mapya na elimu ya juu,” alisema Rais Ruto.

Kiongozi wa taifa aliyasema hayo siku ya Ijumaa, wakati wa sherehe ya kufuzu kwa maafisa wa vikosi vya ulinzi katika chuo cha ulinzi cha Kenya kilichoko Lanet, kaunti ya Nakuru.

Rais alitoa changamoto kwa maafisa hao waliofuzu kuboresha ujuzi wao kwa kushirikiana na wataalam  wa nyanja mbali mbali.

“Hatua hiyo ndiyo itakuwezesha kuafikia ufanisi katika mazingira yaliyosheheni changamoto,” alidokeza kiongozi huyo wa nchi.

Aidha Rais Ruto alisema serikali inatekeleza mfumo wa kuimarisha uchumi wa Bottom Up, ili kuwapa uwezo wananchi kwa lengo la kuwaepusha kujihusisha na shughuli haramu ambazo huenda zikayumbisha taifa.

“Tunafahamu kuwa hali ya umaskini ni chanzo cha vijana kujiingiza katika shughuli za uvunjaji sheria,” alisema Rais Ruto.

Vyeti mbalimbali vya shahada na stashahada vilitolewa kwa waliofuzu katika hafla hiyo.

Aidha hafla hiyo ilihudhuriwa na mkuu wa vikosi vya ulinzi nchini Francis Ogolla, waziri wa Ulinzi Aden Duale, Gavana Susan Kihika miongoni mwa wengine.

Share This Article