Ruto: Serikali kubadili jina la Tume ya Kudumu ya Muziki ya Rais

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais William Ruto.

Rais William Ruto amedokeza kuwa serikali ina mipango ya kubadilisha jina la Tume ya Kudumu ya Muziki ya Rais (PPMC).

Akizungumza Jumatano wakati wa tamasha ya kitaifa ya muziki katika ikulu ya Nakuru, Rais alisema tume hiyo sasa itajulikana kama Tume ya Ubunifu ya Kenya.

Kiongozi wa taifa alisema tayari mswada umetayarishwa na utawasilishwa bungeni katika muda wa miezi miwili ijayo ili kuhalalisha mchakato huo.

“Nimemuagiza Waziri Ababu Namwamba kuwa mswada huo uwasilishwe bungeni katika muda wa miezi miwili, ili tutoe fursa ya kukuza talanta,” alisema Rais Ruto.

Aliongeza kuwa mswada huo utahakikisha tume hiyo ya ubunifu, inakuwa na studio za kisasa sio tu Nairobi lakini katika kila kaunti hapa nchini.

Rais Ruto alitumia hafla hiyo kutuliza wasiwasi ulioibuka kuhusu maudhui yasiyofaa katika mtandao wa Tiktok,  akisema atakutana na afisa mtendaji wa mtandao huo ili kuzungumzia suala hilo.

Share This Article