Rais William Ruto amesema Serikali imejitolea kuimarisha uzalishaji wa kilimo nchini kwa kuwapiga jeki wakulima kuzalisha zaidi.
Kiongozi huyo wa mataifa alidokeza kuwa madhumuni hayo ni kuafikia malengo ya usalama wa chakula, kupunguza gharama za maisha na uagizaji wa chakula kutoka nje, kuongeza mauzo ya nje na kubuni ajira katika msururu wa kuongeza thamani kwa bidhaa za kilimo.
“Katika miaka mitano ijayo, tunataka kupunguza pesa tunazotumia kuagiza chakula kutoka nje kwa asilimia 50, na hivyo kuokoa Shilingi bilioni 250. Katika miaka 10, tunataka kusitisha uagizaji wa bidhaa zote za chakula kutoka nje,” alisema.
Ili kufanikisha hili, Rais Ruto alisema Serikali imepunguza gharama ya uzalishaji, akitaja utoaji wa mbolea ya bei nafuu kama mfano.
Zaidi ya hayo, Rais alisema Serikali inajenga mabwawa ili kupunguza utegemezi mkubwa wa nchi kwenye kilimo cha kutegemea mvua.
“Tunataka kuongeza mazao yetu ya kilimo kwa kuwasaidia wakulima wetu kupata mbegu bora, mbolea ya bei nafuu na maji kwa ajili ya umwagiliaji,” alisema.
Naibu wa Rais Rigathi Gachagua alipongeza uongozi thabiti wa Rais Ruto ambao umesababisha uchumi wa nchi kuimarika na mzigo wa madeni kudhibitiwa.
Aliwataka Wakenya kumuunga mkono Rais na kuunga mkono mipango ya Serikali inayolenga kubadilisha maisha yao.
Mawaziri Alice Wahome, Moses Kuria, Eliud Owalo, Ezekiel Machogu na Mithika Linturi, Gavana wa Meru Kawira Mwangaza na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wa walihudhuria.
Viongozi wengine walikuwa Seneta Kathuri Murungi (Meru), Wabunge Elizabeth Karambu (Meru Women Rep), Mpuru Aburi (Tigania Mashariki), John Paul Mwirigi (Igembe Kusini), Rindikiri Mugambi (Buuri), John Mutunga (Tigania Magharibi), Shadrack Mwiti (Imenti Kusini), Moses Kirima (Imenti ya Kati) na Dorothy Muthoni (Aliyeteuliwa), miongoni mwa wengine.