Rais Ruto: Serikali itashirikiana na sekta ya kibinafsi kubuni nafasi za ajira

Tom Mathinji
2 Min Read

Zaidi ya vijana 3,500  kutoka kanda ya Afrika ya mashariki wamenufaika na kozi mbali mbali chini ya mpango wa 2jiajiri unaofadhiliwa na benki ya KCB kwa ushirikiano na GIZ E4D Kenya.

Akizungumza wakati wa hafla ya kufuzu kwa vijana 3,500 chini ya mpango huo katika uwanja wa michezo wa Kimataifa wa Moi Kasarani, Kaunti ya Nairobi, Rais William Ruto, alisema mpango wa Wakfu wa KCB unalenga kusaidia vijana kukuza biashara ndogo ndogo kwa kuwapa ujuzi wa utendakazi.

Alibainisha kuwa Serikali itashirikiana na sekta binafsi katika kubuni nafasi zaidi ya 100,000 za uanagenzi.

Alieleza kuwa sekta binafsi itapewa vivutio vya kuifanya isaidie mpango huo.

“Iwapo [sekta ya kibinafsi] itawalipa wafanyikazi Shilingi 25,000 kwa mwezi, Serikali itawarudishia Sh12,000,” alisema Dkt Ruto.

Rais alisisitiza kuwa Serikali imechukua hatua za makusudi kubuni fursa za ajira kwa vijana mara wanapo kamilisha mafunzo yao.

Alieleza kuwa Serikali inabuni fursa katika mpango wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu, ujumuishaji wa kaunti na maeneo ya viwanda, uchumi wa kidijitali na maeneo maalum ya kiuchumi, miongoni mwa mengine.

“Lengo ni kupunguza umaskini na ukosefu wa usawa, na kuzalisha utajiri kwa Wakenya,” alisema.

Rais Ruto alisema kuwa Serikali imeshughulikia changamoto za ufadhili wa Taasisi za Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVETs) ili kuimarisha taasisi hizo.

“Tumeongeza maradufu bajeti ya TVET zetu ili tuweze kupanua fursa zaidi za kupata ujuzi wa kiufundi,” alisisitiza.

Alisema Serikali pia itajenga TVETS mpya 15 na kuajiri wakufunzi 17,000.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *