Rais William Ruto amesema serikali ya Kenya imejitolea kulipa madeni yake, huku ikiendeleza mipango ya kukuza uchumi wa taifa hili.
Akihutubia taifa katika bunge la pamoja la kitaifa na lile la Seneti, kiongozi wa taifa alisema serikali italipa dola milioni 300 ambayo ni sehemu ya deni la Eurobond la dola bilioni mbili.
Katika hotuba hiyo ya Rais ambayo ni yake ya kwanza tangu alipochukua hatamu za uongozi, Ruto alielezea matumaini kwamba taifa hili litalipa madeni yake, swala alilosema liliibua wasiwasi miongoni mwa wakenya, washirika na masoko, katika hatua aliyoitaja ya kukuza uchumi wa Kenya.
“Nawafahamisha kwa ujasiri kuwa tutalipa madeni ambayo yameibua wasiwasi miongoni mwa wakenya na washirika wetu,”alisema Rais Ruto.
Rais Ruto alisema juhudi zinazotekelezwa na taifa hili, zimeimarisha uhusiano mwema na shirika la fedha duniani IMF, benki ya dunia, benki ya maendeleo ya Afrika na washirika wengine wa kimaendeleo katika kuboresha mpango wa kiuchumi wa Bottom-up.
Alisema ukuaji wa biashara zile ndogo na za kadri zilidumazwa na mzigo mkubwa wa madeni, huku watu wengi na hata biashara zikiorodheshwa katika taasisi ya CRB.