Rais Ruto: Serikali itaboresha maeneo yanayokumbwa na ujangili

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais Ruto afanya ziara katika kaunti ya Baringo.

Serikali imedhamiria kubadilisha sura ya Kerio Valley na maeneo mengine ya Kenya ambayo kwa muda mrefu yamekumbwa na ujambazi na aina zingine za ukosefu wa usalama, Rais William Ruto amesema.

“Tutabadilisha sura ya Tiaty, Kaunti ya Baringo, mikoa mingine ya Kerio Valley na maeneo yote yaliyotengwa ili watoto wetu wote wapate fursa sawa,” Rais Ruto akadokeza.

Alitaja kuzinduliwa kwa vyuo vya KMTC na TVET kama baadhi ya mipango ambayo serikali ilikuwa ikifuatilia kubadilisha maeneo yaliyotengwa nchini Kenya.

“Mpango wetu ni kuwekeza katika maeneo haya ili  Kenya isonge mbele kwa usawa,” alieleza.

Rais alitoa mfano wa uwekezaji katika mradi wa jotoardhi wa Silale, akisema utatengeneza ajira kwa vijana na kubadilisha mtindo wa maisha wa watu wa eneo hilo.

Rais Ruto alizungumza siku ya Ijumaa katika ziara ya maendeleo katika Kaunti ya Baringo.  Alikagua ujenzi wa Chuo cha Mafunzo haya Ufundi cha Bonde la Ufa Kaskazini na kufungua Maabara ya Ujuzi wa Dijitali ya Konza ya taasisi hiyo katika Eneo Bunge la Tiaty.

Pia alizindua Chuo cha Mafunzo ya Matibabu cha Kenya huko Chemolingot na kutoa hati miliki kwa zaidi ya watu 2,530.

Rais aliandamana na Magavana Benjamin Cheboi (Baringo), Wisely Rotich (Elgeyo Marakwet), wabunge na Wawakilishi wa Wadi kadhaa.

Rais Ruto alibainisha kuwa ukuzaji wa nishati ya jotoardhi huko Baringo ni uwekezaji mkubwa ambao utavutia wawekezaji katika utengenezaji wa bidhaa za kijani na kuiweka kaunti hiyo kama kitovu kikuu cha utengenezaji nchini Kenya.

Share This Article