Rais William Ruto alielezea kutekelezwa mabadiliko ya mpango wa afya aliposhauriana na vijana Ijumaa kupitia mtandao wa X.
Kiongozi huyo wa taifa alihakikishia kuwa atashughulikia tatizo la ajira ya Madaktari wanagenzi.
“Nilikutana na viongozi wa madaktari na tulikubaliana kulipa na kukamilisha malimbikizi yao kabla ya mwisho wa mwaka huu,” alisema Rais.
Kuhusu mpango wa bima ya afya kwa wote UHC, Rais alisema serikali imeongeza ufadhili kwa mpango huo akitoa mfano wa kuimarishwa kwa mpango wa Linda Mama.
“Chini ya mpango wa UHC, tumeongeza bima hiyo hadi shilingi 11,200 huku bima ya kujifungua kwa kina mama kupitia upasuaji ikiongezwa hadi shilingi 32,200,” aliongeza Rais.
Alisema hazina ya bima ya afya kwa wote (SHIF) itahakikisha kila mkenya anapata bima ya matibabu.
Aliongeza kuwa kupitia mipango ya kidijitali shughuli ya utoaji huduma za afya zitaiwianishwa katika vituo vya umma na vya kibinafsi na hivyo kuondoa desturi ya uchangishaji kwa minajili ya kukidhi ada ya matibabu.
Alitoa wito kwa wakenya kumakinika na mbinu za kupanga afya yao.