Serikali imejitolea kuhakikisha ugatuzi unafanikiwa, ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi. Hayo ni kwa mujibu wa Rais William Ruto.
Rais alisema utawala wa Kenya Kwanza unafanya kazi na magavana wote, bila kujali misimamo yao ya kisiasa, kwa lengo la kuchochea ukuaji na maendeleo jumuishi.
Aidha alikubali vitengo vilivyogatuliwa kuwa mali muhimu katika utekelezaji wa ajenda ya mabadiliko ya kiuchumi ya Kutoka Chini kwenda juu almaarufu Bottom Up.
Alitaja mpango wa nyumba za bei nafuu kuwa miongoni mwa mipango ambayo ngazi zote mbili za serikali zinashirikiana kutekeleza.
“Tunaziona serikali za kaunti kama rasilimali na washirika katika utekelezaji wa mpango na mabadiliko ya nchi yetu,” alisema.
Aliyasema hayo siku ya Jumanne wakati wa mkutano wa pamoja uliohudhuriwa na uongozi wa baraza la magavana, ukiongozwa na Mwenyekiti Ann Waiguru mjini Naivasha, Kaunti ya Nakuru.
Rais alisema amewaalika viongozi wa baraza la magavana kwenye kikao hicho cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa ili kuimarisha ushirikiano kati ya ngazi hizo mbili za serikali.
Aliwataka wanachama wa Serikali Kuu kufanya kazi kwa karibu na serikali za kaunti katika utekelezaji wa majukumu yao, akisema haitakuwa na tija kuwaweka kando.
“Lazima tuunganishe mawazo na mipango yetu ili kwa pamoja tuweze kubadilisha nchi yetu,” aliongeza.
Aliwapongeza magavana kwa kuwa na ushirikiano.
Kwa upande wake, Gavana Waiguru alisema ushirikiano kati ya serikali ya Kitaifa na ile ya kaunti umekuwa na athari kubwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Angalia mambo ambayo tumefanikiwa katika afya tulipofanya kazi kwa ushirikiano na kukutana nusu mbali. Ikiwa tutafanya vivyo hivyo na majukumu mengine yaliyogatuliwa, tutafaulu mengi zaidi, “aliongeza.