Rais Ruto: Niliungana na Raila kwa ajili ya umoja wa taifa

Rais William Ruto na kinara wa chama cha ODM Raila Odinga walitia saini makubaliano ya kisiasa Ijumaa wiki iliyopita. Wote hao wanasema makubaliano hayo yamekusudia kuwaunganisha Wakenya.

Martin Mwanje
1 Min Read
Rais William Ruto wakati akiwahutubia wakazi wa Kamukunji, kaunti ya Nairobi

Rais William Ruto ametetea hatua yake ya kuungana na kinara wa chama cha ODM Raila Odinga akisema lengo lake kuu ni kuwaunganisha Wakenya. 

Ruto na Raila Ijumaa wiki iliyopita walitangaza azimio la kuzika tofauti zao na kufanya kazi pamoja kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

“Si mliona juzi, tumekubaliana na Mheshimiwa Raila Odinga, tukasema tuunganishe Kenya. Tuwache ubaguzi, tuwache chuki, tuwache ukabila,” alisema Rais Ruto wakati akiwahutubia wakazi wa Kamukunji, kaunti ya Nairobi leo Jumatatu alikozindua miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Kenya ni nchi moja. Sisi wote ni watu wa taifa moja, with a common destiny. Nairobi mnasema ndio au mnasemaje?”

Matamshi sawia yametomewa na Raila ambaye ametetea hatua yake ya kufanya kazi na Rais Ruto akisema haikuchochewa na maslahi ya kibinafsi.

Kinyume cha wakosoaji wake, Raila anasema aliweka mbele maslahi ya kuliunganisha taifa kuliko yake mwenyewe katika kuungana na Rais Ruto kulitumikia taifa.

Viongozi wa upinzani wakiongozwa na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka wamemnyoshea Raila kidole cha lawama wakimtaja kuwa msaliti.

Aidha, wamedai hatua ya Raila ilichochewa na maslahi ya kibinafsi wala si ya kitaifa.

Upinzani umeapa kuhakikisha utawala wa Kenya Kwanza unatemwa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Website |  + posts
Share This Article