Rais William Ruto amesema atajibidiisha kulinda rasilimali za umma.
Amesema hali itakuwa si hali tena kwa watumishi wa umma wenye tabia ya kutumia vibaya rasilimali za umma.
Kiongozi wa nchi amesikitika kwamba umekuwa mtindo kwa baadhi ya watu kufanya kazi katika afisi za umma ili kuiba.
Amesisitiza kuwa ufisadi ni sharti ukomeshwe, hasa katika utoaji zabuni.
“Hatutasubiri hadi fedha zipotee. Tutashughulikia hilo punde tukitambua dalili zake.”
Alisisitiza kuwa hakutakuwa na fedha za kuiba bali za kutimiza mipango ya serikali.
Ruto amewataka watumishi wa umma kuwa wahudumu badala ya wakuu wa watu.
Ameonya kuwa utepetevu hautakubaliwa.
“Ni lazima tufanye kazi kwa bidii na kwa njia bora ili kutimiza ahadi zetu. Tuna fursa ya kubadilisha nchi yetu.”
Rais aliyazungumza hayo wakati wa kutiwa saini kwa Kandarasi za Utendakazi za Kiwizara za Mwaka 2023/2024 katika Ikulu ya Nairobi.
Naibu Rais Rigathi Gachagua, Waziri Mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, Mawaziri na Magavana ni miongoni mwa waliokuwapo.
Rais Ruto alielezea kuwa serikali imeazimia kuboresha utendakazi wake kwa kujumuisha utekelezaji wa Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi kutoka Watu wa Tabaka la Chini hadi Juu kwa utiaji saini kandarasi za utendakazi.
“Madhumuni yetu ni kufikia viwango vya juu zaidi vya utendakazi katika kutoa huduma kwa umma.”
Alisema hili litafanyika kupitia uwajibikaji na utumiaji wa rasilimali za umma kwa uwazi.
Naibu Rais Rigathi Gachagua aliwataka watumishi wa umma kuwa na ari ya kuwatumikia raia akiongeza kuwa hakuna muda wa kupoteza.
“Urafiki wetu utajikita tu kwa utendakazi. Hebu tufanye kazi na tufanye tunachopaswa kuwafanyia Wakenya,” alisema Gachagua.
Kwa upande wake, Mudavadi alisema kuna haja ya kulainisha usimamizi wa utendakazi katika sekta ya umma.
Alisema hii itasaidia katika upangaji, utengenezaji bajeti na utendakazi.
“Mabadiliko ya sekta ya umma ni lazima yafuatwe ili kuibadilisha sekta ya umma na kubuni mazingira ambayo yataboresha utendakazi,” alisema Mudavadi.