Rais William Ruto na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, UN António Guterres, watazindua rasmi mradi wa upanuzi wa Umoja wa Mataifa jijini Nairobi leo Jumatatu.
Mradi wa Gigiri, uliopitishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa Disemba 2023, utagharimu dola milioni 340 za Marekani sawa na shilingi bilioni 43.8 za Kenya.
Mradi huo unahusisha uboreshaji mkubwa wa vifaa vya mikutano katika afisi za Umoja wa Mataifa za Nairobi kwa gharama ya dola milioni 265.6 za Marekani sawa na shilingi bilioni 34.3 za Kenya na ukarabati wa majengo ya ofisi kwa gharama ya dola milioni 74.5 za Marekani sawa na bilioni 9.6 za Kenya.
Leo Jumatatu, Ruto na Guterres wataweka jiwe la msingi kwa ajili ya jengo jipya la mikutano na kuzindua majengo ya kisasa ya ofisi yaliyokamilika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa katika eneo la Gigiri, Nairobi.
Akiwa Nairobi, Guterres pia atafanya mazungumzo ya ngazi ya juu na viongozi wa Kenya na kushiriki mijadala ya kikanda, ikiwemo mkutano wa Africa Forward unaoandaliwa kwa pamoja na Kenya na Ufaransa.
Mradi huo, uliopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2023, unatarajiwa kugeuza Nairobi kuwa moja ya vituo muhimu zaidi vya kimataifa vya Umoja wa Mataifa duniani.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa Nairobi, Bi. Zainab Hawa Bangura, amesema kuwa mradi huo ni hatua muhimu sana kwa Umoja wa Mataifa barani Afrika.
“Uwekezaji huu unaendana na uhalisia wa sasa ambapo changamoto za kimataifa, pamoja na suluhisho zake, zinazidi kujikita hapa” alisema Bangura.
Aliongeza kusema kwamba Nairobi sio tu mwenyeji bali ni kituo cha kimkakati cha kutekeleza kazi za Umoja wa Mataifa katika karne ya 21.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kupitia azimio nambari 78/253, lilitoa idhini ya mabadiliko yatakayowezesha maendeleo ya miundombinu katika eneo la UNON huko Gigiri.
Upanuzi wa Nairobi umesababisha mashirika kama United Nations Children’s Fund (UNICEF), United Nations Population Fund, na UN Women kuhamishia baadhi ya shughuli zao za kimataifa Nairobi.
Hata hivyo, makao makuu ya mashirika hayo yataendelea kubaki New York.