Serikali itajenga masoko mapya 10 katika kaunti ya Nyandarua mwaka huu wa fedha.
Rais William Ruto amesema masoko hayo yatakuwa sehemu bora ya wafanyabiashara wadogo wadogo kuendesha biashara zao.
“Mazingira mwafaka yatafanya wajasiriamali kujipatia kipato zaidi kutokana na kazi zao,” alisema Rais Ruto.
Alizungumza hayo leo Alhamisi katika mji wa Shamata, eneo bunge la Ndaragwa alikozindua uwekaji lami kwenye barabara ya Maili Kumi – Kariamu, Warukira-Shamata na na ile ya Mairo Inya – Salama.
Alielezea kuwa uwekaji lami kwenye babara hizo zenye urefu wa zaidi ya kilomita 400 katika kaunti ya Nyandarua utawahakikishia wakulima mazingira mwafaka ya mazao yao.
“Miundombinu iliyoboreshwa inamaanisha mapato bora, ajira zaidi na ukuaji zaidi wa nchi yetu.”
Naibu Rais Rigathi Gachagua, Gavana Moses Badilisha na wabunge wakiongozwa na mwenyeji wao George Gachagua walikuwapo.
Aidha Rais alisema kuwa uboreshaji wa barabara hizo utapunguza gharama za usafirishaji na hasara za baada ya mavuno.
Aliongeza kuwa ni mpango wa serikali kufufua kilimo ambacho kwa muda mrefu kimekuwa uti wa mgongo wa nchi hii kiuchumi.
Kwa upande wake, Gachagua alisema serikali itaendelea kubuni na kupanua fursa za kiuchumi ili kuwawezesha vijana kujiendeleza.