Rais Ruto: Mashindano ya WRC yataimarisha uchumi wa taifa

Tom Mathinji
2 Min Read

Serikali inalenga kutumia vyema Mashindano ya Dunia ya Mbio za Magari (WRC) ili kutanua fursa za kiuchumi nchini.

Rais William Ruto amesema mashindano hayo yanavutia zaidi ya wageni 100,000 na kubuni nafasi za kazi zenye thamani ya shilingi bilioni 24.7.

Kando na kubuni nafasi za ajira, hafla hiyo itakuza sekta ya utalii.

Rais alisema mashindano hayo yameipa Kenya umaarufu duniani kupitia vyombo vya habari wenye thamani ya shilingi bilioni  nane na thamani ya jumla ya kiuchumi ya shilingi bilioni 63.3.

“Hii itaifanya Kenya kujulikana kama taifa tajika la michezo, bingwa wa mashindano ya magari na kivutio cha utalii.”

Alizungumza hayo jana Jumatano alipoanzisha rasmi mashindano ya magari ya Safari Rally mjini Naivasha, kaunti ya Nakuru.

Hafla hiyo ilivutia makundi 34 kutoka nchi 20.

Rais aliwapongeza waandaaji wa WRC kwa mpango wao wa kupanda miti unaoitwa ‘Greening Legacy Programme’ unaoazimia kupanda miti milioni 19.

Aliwasihi waandaaji wa mashindano hayo kuendeleza mchezo huo na kuhakikisha uendelevu kwa kuhimiza ukuzaji wa vipaji.

“Tunataka kuona safu ya ukuzaji yenye vipaji kama vya hapo awali ikiongozwa na Joginder Singh, Peter Hughes, Nick Norwicki, Shekhar Mehta, Vic Preston Senior na Junior,” alieleza.

Gavana wa kaunti ya Nakuru Susan Kihika, Waziri wa Michezo Ababu Namwamba na Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa KCB Paul Ruso ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria hafla hiyo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *