Rais William Ruto atazindua rasmi azima ya Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga ya kuwania wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC.
Hii ni kulingana na Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi aliyetoa taarifa baada ya kufanya majadiliano na Raila.
Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje alisema uzinduzi huo utafanyika Agosti 27, 2024 huku uchaguzi wa mwenyekiti wa AUC ukitarajiwa kuandaliwa mwezi Februari mwakani.
Raila alisema amezuru nchi mbalimbali barani Afrika ambapo amekutana na viongozi waliodhihirisha matumaini kuhusu umoja wa Afrika.
Kulingana naye, Umoja wa Afrika unastahili kuboreshwa ili uwezeshe raia wa nchi za Afrika kuafikia ndoto za waanzilishi za umoja, amani na ufanisi.
Mudavadi alisifia Raila kama mwaniaji wa Kenya wa wadhifa huo akisema ana tajriba ya kushikilia wadhifa huo na amejitayarisha vyema kushiriki mjadala utakaopeperushwa moja kwa moja wa kujadiliana na watu wa Afrika kuhusu namna ya kuendeleza bara hili.
Huku akihimiza Wakenya kumuunga mkono Raila, Mudavadi alisema, “Tumekuwa tukija pamoja kuunga mkono wenzetu katika riadha, michezo na katika majukwaa ya kimataifa. Jinsi tulivyoshabikia wanariadha wetu kwenye michezo ya Olimpiki, tumuunge mkono Raila.”