Rais Ruto kutia saini kuwa sheria mswada wa nyumba za gharama nafuu

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais William Ruto akagua ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika kaunti ya Bomet.

Rais  William Ruto siku ya Jumatatu atatia saini kuwa sheria mswada wa ujenzi wa nyumba za gharama  nafuu, baada ya bunge la taifa kuupitisha sheria hiyo.

Akizungumza katika eneo la Chepalungu kaunti ya Bomet, Rais  Ruto alisema atatia saini mswada huo kuwa sheria ili kuwezesha kutozwa kwa ushuru wa nyumba za gharama nafuu wa asilimia 1.5.

“Jumatatu naenda kuweka sahihi sheria mpya ya nyumba za gharama nafuu, ndio tuhakikishe ya kwamba tumeweka msingi dhabiti,” alisema Rais Ruto.

Alisema mpango wa ujenzi wa nyumba hizo za gharama nafuu utatoa nafasi za ajira kwa vijana nchini  pamoja na kuhakikisha kuna ardhi  ya kutosha kwa kilimo.

“Tutahakikisha ya kwamba kufikia mwaka ujao, vijana 300,000 watakuwa wanafanya kazi katika mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu,” aliongeza kiongozi wa taifa.

Mnamo mwezi Novemba mwaka 2023, mpango huo wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu ulipata pigo, baada ya Mahakama Kuu kusema ushuru wa mradi huo unaotozwa wakenya ni kinyume cha katiba.

Kulingana na mahakama hiyo, matozo hayo yalikiuka kifungu cha 10, 2 (a) cha Katiba ya Kenya.

Katika ziara hiyo ambapo Rais alikagua ujenzi wa nyumba 220 za gharama nafuu zinazojengwa katika eneo bunge la Chepalungu, kiongozi wa taifa aliandamana na naibu wa Rais Rigathi Gachagua, Waziri wa Barabara Kipchumba Murkomen na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah.

TAGGED:
Share This Article