Rais William Ruto siku ya Ijumaa, atashiriki meza ya mazungumzo na vijana katika mtandao wa X kuanzia saa nane alasiri.
Kulingana na Ikulu ya Rais, baraza la mawaziri pia litajiunga katika majadiliano hayo yatakayochukua muda wa saa tatu.
Hatua hiyo inajiri kufuatia maandamanao yaliyodumu wiki tatu, yaliyoandaliwa na vijana almaarufu Gen Z, wakishinikiza mabadiliko serikalini.
Tangazo hilo lilitolewa kupitia taarifa kwa vyombo vya habari baada ya mkutano wa baraza la mawaziri, ulioongozwa na Rais William Ruto leo Alhamisi.
Wakenya wamealikwa kushiriki mazungumzo hayo yatakayoanza saa nane alasiri hadi saa kumi na moja jioni.
“Wakenya wote wanaalikwa kushiriki katika mazungumzo hayo, kwa lengo la kufanya taifa hili liwe bora zaidi kwa kila mmoja,” ilisema taarifa hiyo.
Vijana walishiriki maandamano kupinga Mswada wa Fedha 2024, na kusaabisha Rais William Ruto kutangaza kuwa hatatia saini kuidhinisha mswada huo,na badala yake ataurejesha bungeni kwa mwongozo zaidi.
Wakati wa mahojiano kwenye runinga Jumapili iliyopita, kiongozi wa taifa alisema yuko tayari kujadiliana na vijana wa taifa hili, kupitia mfumo wanaoupendelea.