Rais William Ruto ataondoka humu nchini leo Alhamisi kuhudhuria mikutano miwili muhimu jijini Kampala, Uganda.
Kupitia kwa taarifa, msemaji wa ikulu Hussein Mohamed, alisema Rais Ruto atahudhuria mkutano wa shirika la IGAD kuhusu ushirikiano wa kanda kuambatana na kujitolea kwa Kenya kwa udhabiti wa kanda ya Afrika mashariki.
Siku ya Ijumaa Rais Ruto atahudhuria kongamano la 19 la mataifa yasiyofungamana na siasa za upande wowote, kuangazia masuala muhimu miongoni mwayo amani duniani na mikakati iliyowekwa baada ya janga la Covid 19.
Kwenye kongamano hilo ambalo kauli mbiu ni kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kiongozi huyo wa taifa, atashiriki katika mjadala kuhusu masuala muhimu yakiwemo mageuzi ya shirika la Umoja wa Mataifa, amani na usalama, malengo ya maendeleo endelevu, mabadiliko ya hali ya anga na mageuzi ya mfumo wa kifedha duniani.
Ruto anatarajiwa kuandaa mikutano kadhaa na marais na viongozi wa nchi za kanda hii, kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kuelezea wajibu wa Kenya katika masuala ya kanda hii na kimataifa.