Rais Ruto kufungua kongamano la uwekezaji Nyanza

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto anatarajiwa kufungua rasmi kongamano la kimataifa la uwekezaji la eneo la Nyanza mwezi ujao, haya ni kulingana na waziri wa mawasiliano na uchumi dijitali Eliud Owalo.

Kongamano hilo la siku mbili litaandaliwa jijini Kisumu Juni 28 na 29, 2024 na linatarajiwa kukutanisha wawekezaji wa humu nchini na wale wa kimataifa.

Owalo alielezea kwamba Rais Ruto ataongoza wawekezaji kutambua fursa za uwekezaji ambazo hazijatumiwa katika kaunti za eneo la Nyanza ambazo ni Kisumu, Homabay, Siaya, Kisii na Nyamira.

Magavana wa kaunti hizo watahudhuria kongamano hilo tayari kutia saini mikataba ambayo huenda ikatikana na kongamano hilo la siku mbili.

Sekta za afya, teknolojia, kilimo na miundombinu ni baadhi ya zile ambazo zitaangaziwa kwenye kongamano hilo ambalo Owalo anasema linawiana na sera ya serikali kuu ya kuendeleza ushirikiano kati ya sekta ya umma na ya kibinafsi.

Waziri Owalo alitaja miradi kama bwawa la Koru-Soin na barabara ya kuunganisha kaunti zilizo karibu na Ziwa Viktoria almaarufu “Lake Victoria ring road” ambayo itaonyeshwa wawekezaji wakati wa kongamano hilo.

Mchoro wa barabara hiyo uko tayari na umeidhinishwa na inapita karibu na Ziwa hilo kutoka kaunti ya Busia hadi kaunti ya Migori. Lengo kuu la barabara hiyo ni kurahisisha biashara na uwekezaji katika eneo la Nyanza na hivyo kutoa nafasi za ajira kwa vijana.

Share This Article