Rais William Ruto leo Ijumaa atasafiri kuelekea mjini Arusha nchini Tanzania kuhudhuria Mkutano usiokuwa wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi wa Afrika Mashariki.
Mkutano huo utawaleta pamoja viongozi wa kanda hii ili kuangazia changamoto kuu zinazoikabili Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC.
Kadhalika, utajadili mikakati ya kuharakisha maendeleo ya pamoja ya kiuchumi, kuimarisha juhudi za kanda za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuangazia ukosefu wa usalama.
“Rais Ruto atapigania kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara, kuimarishwa kwa biashara za kuvuka mpaka na kuongezwa kwa ushirikiano katika nyanja za nishati, kilimo na ubunifu wa kidijitali ili kubuni nafasi za ajira na kuongeza vyanzo vya mapato,” amesema msemaji wa Ikulu ya Nairobi Hussein Mohamed katika taarifa.
“Viongozi pia watazungumzia hatua za kupigia chapuo amani na usalama, ikiwa ni pamoja na kukabiliana na uhalifu wa kimataifa, kusimamia mipaka na kutatua migogoro.”
Leo Ijumaa alasiri, Rais Ruto atashiriki kikao cha kuadhimisha miaka 25 tangu kuasisiwa kwa EAC.
Aidha, Rais atafanya mazungumzo ya pande mbili na viongozi wa kanda hii pembezoni mwa mkutano huo.