Jioni ya Jumanne Agosti 22, 2023, Rais William Ruto ataongoza hafla ya kuanzisha mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu katika eneo bunge la Bahati katika kaunti ya Nakuru.
Mradi huo ni sehemu ya mpango wa serikali wa kuhakikisha kwamba inajenga nyumba za bei nafuu zipatazo laki 2 kwenye maeneo tofauti ya nchi.
Nyumba hizo 220 zitajengwa kwenye ardhi ya ukubwa wa ekari 10 kwa gharama ya shilingi milioni 505.
Kutakuwa na nyumba za chumba kimoja 60, nyumba za chumba kimoja cha kulala 20, nyumba 120 zenye vyumba viwili vya kulala na nyingine 20 zenye vyumba vitatu vya kulala.
Barabara za eneo hilo la makazi zitatengenezwa, umeme kuwekwa humo na mfumo wa kuondoa maji taka utaboreshwa zaidi ya ulivyo kwa sasa.
Vitu vingine ambavyo vitakuwepo kwenye eneo hilo la makazi ni ukumbi wa mikutano, eneo la kuchezea, eneo la kufanyia biashara na eneo la kukuza miche ya miti.
Uzinduzi wa mradi huo unafuatia uzinduzi wa mradi sawia wiki moja iliyopita katika eneo bunge la Gichugu kaunti ya Kirinyaga.
Katibu wa Ujenzi wa Nyumba na Maendeleo ya Miji Charles Hinga anasema ujenzi wa nyumba za bei nafuu sio wa kufaidi kaunti ya Nairobi pekee bali unalenga maeneo bunge yote humu nchini.
Kufikia sasa, serikali imetoa zabuni 17 za ujenzi wa nyumba za bei nafuu kwenye awamu ya kwanza na kutangaza zabuni nyingine 35 katika awamu ya pili.