Rais Ruto kuanza ziara ya siku 5 Mlima Kenya

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto wiki hii hadi wiki ijayo amepangiwa kuanza ziara ya maendeleo katika eneo la Mlima Kenya. 

Ziara hiyo ya siku tano itaanza Jumamosi asubuhi akisafiri kutoka Nairobi kwa kutumia barabara na kusimama katika maeneo ya Githurai na Kenol.

Akiwa katika kituo cha biashara cha Kagio, Rais Ruto anatarajiwa kufungua mradi wa maji kabla ya kuwahutubia raia katika eneo la Baricho katika kaunti ya Kirinyaga.

Akiwa Karatina, kiongozi wa nchi atazindua ujenzi wa barabara ya Marua kuelekea Ikulu Ndogo ya Sagana ambayo itarahisisha usafirishaji wa bidhaa na utoaji huduma na kuchochea ukuaji wa eneo hilo.

Siku ya Jumapili, atahudhuria ibada katika Ikulu Ndogo ya Sagana.

Jumatatu ijayo, Rais ataelekea katika eneo la Mukurweini ambako atazindua ujenzi wa barabara.

Kisha atakuwa mwenyeji wa viongozi wa Mlima Kenya katika Ikulu Ndogo ya Sagana ambako masuala ya kilimo, miundombinu na elimu miongoni mwa mengine yanatarajiwa kujadiliwa.

Magavana, wabunge na Wawakilishi Wadi ni miongoni mwa wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo.

Ziara ya Rais inatarajiwa kukamilika Jumatano wiki ijayo atakapofungua hospitali ya Naromomoru Level IV na kisha kuzindua mradi wa nyumba za bei nafuu katika eneo la Gichugu miongoni mwa shughuli zingine.

Eneo la Mlima Kenya linachukuliwa kuwa ngome ya kisiasa ya utawala wa Kenya Kwanza baada ya utawala huo kujizolea mamilioni ya kura kutoka eneo hilo wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *