Rais William Ruto amesema serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha kuwa kila eneo bunge hapa nchini lina chuo cha mafunzo ya kiufundi, TVET katika muda wa miaka miwili ijayo.
“Tuna vyuo 24 vya kiufundi kote nchini, 13 kati ya hivyo viliboreshwa hivi karibuni, na vyuo vya ufundi 272, na 16 vimepangwa kukamilika katika mwaka wa fedha wa 2024/2025,” alisema Rais Ruto.
Akizungumza siku ya Jumanne wakati wa sherehe za miaka 100 ya taasisi za TVET hapa nchini katika kaunti ya Nyeri, kiongozi wa taifa alisema mwaka huu wa fedha, serikali imetenga shilingi bilioni 28.3 kwa taasisi za TVET.
“Tunakusudia kuendelea kuongeza mgao wa bajeti katika siku zijazo hadi tufikie kiwango bora cha uwekezaji.”
Ruto aliongeza kuwa serikali pia inaajiri wakufunzi 2,000 wa TVET, kwa lengo la kuongeza idadi hiyo hadi 4,000.
Rais alitangaza kuwa China imeidhinisha shilingi bilioni 13 kwa Kenya kusaidia taasisi 70 za TVET kuwa na vifaa vya kisasa.
“Tuna nia ya dhati ya kuwatambulisha vijana wetu kwa ujuzi, maarifa na teknolojia bora zaidi ulimwenguni,” Rais alisema.
Kuhusu vituo vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) vinavyojengwa katika wadi 1,450 nchini na taasisi za TVET kote nchini, Rais Ruto alisema mafunzo hayo yanawapa vijana ujuzi muhimu unaowapa fursa mpya mtandaoni.
Rais Ruto alisema: “Tunataka kuhakikisha kuwa tunatumia nafasi ya kidijitali na vijana wetu wenye talanta kuendesha uchumi wetu kupitia kazi za kidijitali.”
Alisema serikali imetia saini mikataba 19 ya wafanyikazi na nchi 19 ili kupanua fursa kwa Wakenya.
Kiongozi wa nchi alisema serikali imejizatiti kupambana na ulevi na matumizi ya dawa za kulevya ambayo, alisema, inazuia ukuaji wa nchi.