Rais Ruto: Kiaraho alikuwa kiongozi mnyenyekevu na shupavu

Tom Mathinji
2 Min Read
Marehemu mbunge wa Ol Kalou David Njuguna Kiaraho.

Rais  William Ruto amemuomboleza marehemu mbunge wa Ol Kalou David Njuguna Kiaraho kuwa mtu mnyenyekevu, shupavu na mwenye maono.

“Nimehuzunishwa na kifo cha David Njuguna Kiaraho. Tunawaombea familia, marafiki na wakazi wa Ol Kalou wakati huu wa kipindi kigumu,” aliomboleza Rais Ruto.

Kiongozi wa taifa alidokeza kuwa David Kiaraho atakumbukwa kwa mchango wake wa kupigiwa mfano katika sekta ya elimu na huduma zake katika Bunge la Taifa.

“Maisha yake yaliwapa wengi motisha katika kizazi hiki kuwa viongozi wasio na uhasama wa kisiasa na kuzingatia lengo la utoaji huduma kwa wananchi,” aliongeza Rais Ruto.

Kwa upande wake, Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki alimuomboleza mbunge huyo kuwa mtu mpole, mwenye heshima na aliyeheshimiwa katika tasnia ya wachoraji ramani.

“Habari za huzuni kuhusu kifo cha David Kiaraho, mbunge wa Ol Kalou, ni kumbukumbu ya jinsi maisha hubadilika,” alisema Kindiki.

Alisema kuwa taifa hili limempoteza kiongozi aliyefanikisha mengi hasaa wakati huu ambapo alihitajika zaidi.

“Familia yake imepoteza msingi, eneo bunge lake limempoteza mwakilishi shupavu na Kenya imepoteza shujaa aliyeafikia mengi, Mungu ailaze roho yake mahali pema,” aliomboleza kindiki.

Kifo cha Kiaraho kilitangazwa rasmi na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetangula, akisema alifariki akipokea matibabu katika Hospitali ya Nairobi Jumapili asubuhi akiwa na umri wa miaka 62.

Share This Article