Kenya itashirikiana na taasisi za fedha za Afrika kwa kuwa zina nafasi ya kutoa suluhu mwafaka kuhusiana na masuala ya miundombinu, siasa, uchumi na jamii katika bara hili.
Rais William Ruto alisema Kenya na Shirika la Fedha la Afrika zinashirikiana kuandaa Mkutano wa Miundombinu ya Madini mwezi Aprili mwaka huu.
Rais Ruto aliyasema hayo leo Alhamisi aliposhiriki meza ya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Afrika, Samaila Zubairu, katika Ikulu ya Nairobi.
Katika mkutano huo, Rais Ruto alisema Kenya itajenga uhusiano ambao ni muhimu katika kuimarisha sekta ya madini nchini na kupanua fursa za uwekezaji, ajira, ukuaji wa kitaifa na ustawi.
“Tutakuza mahusiano ambayo ni muhimu katika kuimarisha sekta ya uchimbaji madini na kupanua fursa za uwekezaji, ajira, ukuaji na ustawi,” alisema Rais Ruto.
Rais Ruto pia aliunga mkono mpango wa shirika hilo wa kuanzisha makao yake makuu ya kikanda jijini Nairobi, akiahidi kufanikisha michakato yote muhimu.