Rais William Ruto amesema taifa hili litatekeleza sera ambazo zitainua hadhi ya nchi hii, ili kuvutia uwekezaji wa hali ya juu.
Kulingana na Rais, hatua hiyo itachochea maendeleo ya nchi na kuboresha maisha ya raia wa taifa hili.
Akizungumza leo Jumatano katika jumba la mikutano ya kimataifa KICC, wakati wa mkutano wa kufanyia marekebisho sera ya kigeni ya taifa, Rais Ruto alisema sera hiyo ya kigeni inaelezea bayana malengo, inatambua maswala ibuka na inapendekeza jinsi ya kukabiliana na changamoto za ulimwengu.
Rais alisema sera ya kigeni ya taifa hili, inapaswa kubuni fursa zaidi za kibiashara na kiuchumi kwa viwanda, kwa lengo la kuimarisha biashara ndogo na za kadri, pamoja na kujumuisha makundi maalum kama vile vijana, wanawake na wanaoishi na ulemavu.
Kiongozi huyo wa nchi alisema Kenya imejitolea kuboresha mchango wake katika utangamano wa kanda hii kupitia mikakati kadhaa ikiwa ni pamoja na utekelezwaji wa makubaliano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kufanikisha uchukuzi huru wa bidhaa, huduma na binadamu.
Alitoa wito kwa wadau wote, wakiwemo wale wa kibinafsi na idara za umma, washirika wa hapa nchini na wa kimataifa, kushirikiana kuhakikisha sera hiyo ya kigeni inatekelezwa kwa ufanisi.