Rais William Ruto amesema kuwa Kenya inazidi kudumisha uhusiano mwema wa kidiplomasia na Singapore.
Akizungumza aliposhiriki mazungumzo na balozi wa Singapore asiye mkazi wa hapa nchini Ernest Kan, Rais Ruto alisema nchi hizo mbili zinaendelea kuimarisha kwa pamoja sekta za biashara, uwekezaji, miundombinu, mageuzi ya dijitali na maendeleo ya nguvukazi.
“Singapore ina nafasi muhimu sana katika safari ya maendeleo ya taifa hili,” alisema Rais Ruto.
Kulingana na Rais Ruto, baadhi ya maswala ambayo Kenya inajifunza kutoka Singapore ni pamoja na ustawi wa viwanda, huku taifa hili linapojizatiti kuwa miongoni mwa mataifa yaliyostawi zaidi ulimwenguni.
Kwenye mkutano huo, balozi huyo aliwasilisha ujumbe kutoka kwa Rais wa Singapore Tharman Shanmugaratnam kwa Rais William Ruto, kabla ya maadhimisho ya 35 ya uhusiano wa mataifa hayo mawili.