Rais Ruto: Kenya inadhamiria kutumia nishati safi

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto ameelezea dhamira ya Kenya kuungana na ulimwengu katika kufanikisha matumizi ya nishati safi. 

Rais Ruto ametaja matumizi ya nishati hiyo kuwa hatua muhimu inayohitajika katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Wakati dunia ikikabiliana na athari kubwa za mabadiliko ya tabia nchi, ni muhimu kwetu kuchukua hatua madhubuti katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira, ukataji wa miti, uchafuzi wa hewa na ongezeko la kutisha la uzalishaji wa gesi chafuzi kwa mazingira,” amesema Ruto.

“Kenya, kama nchi zingine duniani, imedhamiria kuhamia kabisa kwenye matumizi jumuishi ya nishati safi kwa kaya zote, kampuni, wazalishaji na walaji. Kiini cha mabadiliko haya ni gesi ya kimiminika, LPG, ambayo ni mbadala safi na bora zaidi kuliko njia za kawaida za nishati za kupikia.”

Rais amesema changamoto  zinazochangia mabadiliko ya tabia nchi zinahitaji kuchukuliwa kwa suluhu za haraka, zilizoratibiwa na bunifu ili kukabiliana na athari za mabadiliko hayo kwa mazingira.

Aliyasema hayo katika shule ya upili ya Jamhuri leo Jumatatu wakati wa uzinduzi wa mpango wa gesi ya kimiminika ya LPG  itakayotumiwa katika taasisi za mafunzo ya umma nchini Kenya.

Viongozi wa dunia wamekuwa wakishinikiza matumizi ya nishati safi kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambazo zimeshuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya dunia.

Athari hizo zinajumuisha ongezeko la joto kali, mvua kubwa zinazosababisha mafuriko na hata ukame ambao umesababisha ukosefu wa chakula kwa mamilioni ya watu.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *