Rais William Ruto amesema uhusiano baina ya Kenya na Ufaransa umekua kwa kasi na kusababisha kunawiri kwa biashara baina ya mataifa hayo mawili.
Chini ya uhusiano huo, Rais Ruto ambaye aliandaa mazungumzo na mwenzake wa Ufarasa Emmanuel Macron jijini Berlin, Ujerumani, alisema mataifa hayo yanakuza ushirikiano wao katika nyanja mbalimbali kama vile miundombinu, mabadiliko ya tabia nchi na juhudi za kutafuta amani katika kanda ya Afrika Mashariki hasa katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Sudan Kusini.
Kiongozi wa taifa alisema Afrika iko tayari kuhakikisha kuwepo wa mazingira bora, kutekeleza mikakati na uwekezaji unaohitajika kutumia maliasili yake kuafikia majukumu yake katika mchakato wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.
Rais Ruto alisema nishati mbadala ndio njia pekee ya kuafikia ustawi wa kudumu chini ya lengo la 7 la Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs kuhusu upatikanaji wa nishati mbadala kwa wote na kuondoa ulimwengu kwenye hatari ya madhara ya mabadiliko ya tabia nchi.
Alisema Afrika ina maliasili ya kutosha kuiwezesha kufungua ukurasa mpya katika juhudi za kuafikia nishati safi kwa bara Afrika na ulimwengu kwa ujumla.