Rais William Ruto leo Jumanne amezindua ujenzi wa kituo cha matibabu ya ugonjwa wa saratani katika eneo bunge la Nyaribari Chache, kaunti ya Kisii.
Akizindua ujenzi huo, kiongozi wa taifa alisema kituo hicho kitakapokamilika, kitasaidia kuhamasisha, kuzuia na kugundua mapema ugongwa wa saratani na kuanzisha matibabu mapema.
“Baada ya kuanzisha mpango wa utoaji huduma za afya kwa wote, tutaangamiza saratani hapa nchini,” alisema Rais Ruto.
Akiwa katika siku ya pili ya ziara yake katika kaunti za Kisii na Nyamira, kiongozi wa taifa anatarajiwa kuzindua na kukagua miradi kadhaa ya maendeleo.
Rais Ruto atazuru hospitali ya Keroka na baadaye kuzindua mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika eneo la Ekambo.
Rais vile vile ataanzisha rasmi ujenzi wa barabara za Sombogo, Marani na Daraja Mbili ili kuimarisha shughuli za uchukuzi kwa wakazi wa eneo hilo.
Jana Jumatatu akiwa katika kaunti ya Nyamira, Ruto alisema shule 68 katika maeneo bunge ya Borabu, Mugirango Kaskazini, Mugirango Magharibi na Kitutu Masaba zitaimarishwa.