Rais Ruto azindua miradi ya maji kaunti za Kakamega na Nandi

Tom Mathinji
3 Min Read
Rais Ruto azindua miradi ya Maji kaunti za Nandi na Kakamega.

Serikali inazidi kufanya maji safi ya kunywa kupatikana kwa Wakenya zaidi, Rais William Ruto amesema. 

Rais pia ameeleza kuwa serikali inatoa miundombinu bora ya usafi wa mazingira hasa katika miji na maeneo mengine ya mijini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa ugavi wa maji na usafi wa mazingira wa Nandi Hills siku ya Jumamosi,  Rais Ruto alisema mradi huo unapanuliwa ili kuongeza idadi ya familia zinazonufaika kutoka 1,000 hadi zaidi ya 10,000.

Alisema mradi huo utafaidika na shilingi milioni 200 kutoka kwa Benki ya Maendeleo ya Afrika na shilingi zingine milioni 140 kutoka kwa serikali.

“Tumejitolea kuhakikisha kuwa Wakenya kote nchini wanapata maji safi ya kunywa,” alisema Ruto.

Wakati huo huo, Rais aliwahakikishia Wakenya kuwa serikali ina nia ya dhati ya kuendeleza miundombinu ya barabara ili kuwawezesha wakulima kusafirisha mazao yao ya shambani hadi sokoni kwa urahisi.

Alisema serikali ya China itafadhili ujenzi wa barabara nchini kwa gharama ya shilingi bilioni 40.

“Nilipozuru China hivi majuzi, Rais wa nchi hiyo alijitolea kufadhili ujenzi wa barabara zetu. Hili litaimarisha juhudi zetu za kuboresha miundombinu yetu,” alidokeza Rais.

Alitangaza kuwa kaunti ya Nandi, kama maeneo mengine ya nchi, imetengewa pesa za mpango wa kuunganisha umeme wa Last Mile. Hazina ya shilingi bilioni 1.5 ya kaunti itaunganisha nyumba 15,000 kwa umeme.

Kuhusu miundombinu ya kidijitali, alibainisha kuwa uanzishwaji wa vituo vya Teknolojia ya Mawasiliano na Habari katika kila Wadi ni sehemu ya juhudi za serikali kubuni nafasi nyingi za kazi za kidijitali kwa vijana.

“Mpango huu utawapa vijana ujuzi wa kidijitali, maarifa na umahiri ambao utawasaidia kuchuma vipaji vyao,” Rais alisema.

Waliohudhuria ni Waziri wa Maji Eric Mugaa, Gavana Stephen Sang na wabunge kadhaa.

Hapo awali, akiwa Namanja katika eneo bunge la Malava, kaunti ya Kakamega, Rais Ruto alizindua Mradi wa Usambazaji Maji wa Vikundi vya Malava ambao hutoa lita milioni 1.2 kila siku.

Mradi huo utahudumia zaidi ya watu 100,000 katika maeneo ya Chemuche, Kabras Mashariki, Kabras Kusini, Shirugu Mugai, Butali Chegulo na Manda Shivanga.

Aliandamana na Mawaziri Wycliffe Oparanya na Eric Mugaa, Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa, wabunge na wawakilishi wadi kadhaa.

Share This Article