Rais William Ruto ametoa wito kwa viongozi kukoma kuwachochea vijana kusababisha vurugu na machafuko nchini.
Badala yake, Ruto amewasihi kuwa sehemu ya suluhu kwa changamoto ya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.
Kiongozi wa nchi amesema uchochezi ambao husababisha vurugu ni hatari siyo tu miongoni mwa vijana bali pia kwa nchi yote kwa jumla.
Amesema serikali yake inatekeleza sera na mipango makusudi inayodhamiria kubuni nafasi za ajira kwa ajili ya vijana.
Alitoa mfano wa mpango wa nyumba za bei nafuu na ajira za dijitali akizitaja kuwa mipango muhimu inayokusudia kubuni nafasi za ajira kwa wanafunzi waliohitimu shule za sekondari, vyuo na vyuo vikuu.
Rais aliyasema hayo alipokutana na Maaskofu, Wachungaji na Wainjilisti kutoka Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili na Kiasili katika Ikulu ya Nairobi leo Jumatano.
Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, vijana 400,000 wamepata ajira ughaibuni kupitia mpango wa kazi sogevu.
Kwa upande wao, viongozi wa kidini waliwashutumu wale wanaopinga ujenzi wa makanisa nchini.