Rais Ruto awasili nchini Rwanda kwa ziara rasmi

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais Ruto awasili nchini Rwanda kwa ziara rasmi.

Rais William Ruto amewasili Kigali, nchini Rwanda kuhudhuria mkutano wa kila mwaka wa maafisa wakuu watendaji wa Bara Afrika.

Rais Ruto anatarajiwa kuwa na shughuli nyingi, ikiwa ni pamoja na mkutano na  wawekezaji, jopo la marais, na mahojiano na gazeti la ‘The Financial Times’ la Uingereza.

Kongamano hilo la kila mwaka la maafisa wakuu watendaji wa Afrika, linatarajiwa kuanza rasmi leo Ijumaa, kwa hotuba ya ufunguzi itakayotolewa na rais wa Rwanda Paul Kagame.

Zaidi ya biashara 2,000 pamoja na watungaji wa sera wamehudhuria, kujadiliana jinsi Afrika inaweza kujikuza kiuchumi duniani.

Kongamano hilo linafungua malango yake dhidi ya msururu wa changamoto za kimataifa. Linawaleta pamoja viongozi watano wa mataifa, mawaziri wakuu wanne, na zaidi ya viongozi wa kibiashara 2,000, maafisa wakuu watendaji pamoja na wawekezaji wa bara Afrika na wale wa kimataifa.

Kongamano hilo pia litaakisi mikakati kabambe, na kutoa mwongozo wa kuimarisha hali ya kiuchumi barani.

Share This Article