Rais William Ruto amewapuuzilia mbali baadhi ya viongozi wa upinzani wanaopinga mpango wa kutoa chanjo kwa mifugo kote nchini.
Mpango huo umepangwa kufanywa mwezi Januari mwakani.
Ruto amesema utoaji chanjo hiyo iliyozalishwa humu nchini utaimarisha afya ya mifugo na uwezo wa kuuza nyama nje ya nchi.
Kulingana naye, mpango huo, unaolenga kuwachanja ng’ombe milioni 22 na mbuzi na kondoo milioni 50, unalenga kukabiliana na maradhi ya kuvuka mpaka kama vile ugonjwa wa miguu na midomo.
Rais Ruto ameelezea kutoridhika na baadhi ya viongozi ambao amewashutumu kwa kupinga miradi ya maendeleo bila sababu za msingi.
Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga Kongamano la 4 la Uongozi la Wafugaji katika kaunti ya Wajir leo Jumanne, kiongozi wa nchi alitoa wito kwa viongozi na wakazi wa kaunti hiyo na maeneo mengine kuunga mkono mpango huo.
“Wale wanaopinga mpango huo hawana sababu na labda hawana ng’ombe. Wakati tunapokuwa na mazungumzo kuhusu ng’ombe, fyata tu ulimi ikiwa hauna ng’ombe,” alisema Rais.
Aliongeza kuwa Taasisi ya Uzalishaji wa Chanjo za Mifugo nchini Kenya (KEVEVAPI) huzalisha chanjo za mifugo ambazo ni salama kwa ng’ombe, kondoo na mbuzi nchini.
Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amekuwa mstari wa mbele kupinga mpango wa kuwachanja mifugo mwezi Januari mwakani akitilia shaka usalama wa chanjo itakayotumika.