Rais William Ruto, amerejelea kujitolea kwake kuunganisha Wakenya, na kutema migawanyiko na siasa za kikabila, akisema siasa za Kenya kamwe hazipaswi kuzingatia misingi ya kikabila.
Akizungumza leo alipozindua tamasha la kitamaduni na kitalii la Turkana mjini Lodwar, Rais alisisitiza haja ya mshikamano wataifa, akidokeza kuwa baraza jumuishi la mawaziri linalenga kuwaunganisha wakenya wote, bila kuzingatia miegemeo yao ya kisiasa.
“Hatutaki siasa za kikabila na za ubaguzi. Tumejitolea kuwaunganisha wakenya na kubuni Kenya yenye ustawi kwa wote,” alisema Rais Ruto.
Tamasha hilo kwa jina Tobong’u Lore, ambayo ni makala ya nane, limenawiri na kuwa hafla kubwa ya kitalii na kitamaduni, ambalo hujumuisha maonyesho ya densi, muziki, vyakula vya kitamaduni na hujumuisha jamii kutoka Kenya, Burundi, Ethiopia, Uganda, na South Sudan.
Rais Ruto alipongeza ushirikiano wa viongozi wa eneo la Pokot Magharibi na Turkana kwa juhudi zao za kukabiliana na changamoto kama vile wizi wa mifugo na ujangili, akihimiza udumishaji umoja na utekelezaji wa maendeleo kwa minajili ya amani.
Aidha kiongozi wa taifa alisema shughuli za kilimo katika eneo la bonde la Kerio, itabadilisha eneo hilo na kuwa kitochu cha chakula, itapunguza uhalifu na kuboresha maisha ya wakazi wa eneo hilo.
“Wakazi wanapojihusisha na ukulima, hakutakuwa na nafasi ya uhalifu katika maeneo ya mipaka,” alisema Rais Ruto.