Rais William Ruto ametia saini kuwa sheria Mswada wa Sukari wa mwaka 2022 unaolenga kufufua sekta ya sukari nchini.
Hafla ya utiaji saini mswada huo imefanyika leo Ijumaa katika Ikulu ya Nairobi. Ilihudhuriwa na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula, Waziri wa Fedha John Mbadi na Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor miongoni mwa maafisa wengine wakuu serikalini.
Mswada huo uliwasilishwa na mbunge wa Navakholo Dkt. Emmanuel Wangwe kwenye Bunge la Taifa na kuchapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali Oktoba 6, 2022.
Katika Bunge la Seneti, uliwasilishwa na Seneta wa Bungoma David Wakoli na kupitishwa baada ya kufanyiwa marekebisho.
Kisha ulirejeshwa na kupitishwa katika Bunge la Taifa Septemba 27, 2023 baada ya kufanyiwa marekebisho.
Lengo kuu la mswada huo ni kuendeleza, kudhibiti na kukuza sekta ya sukari baada ya kubatilishwa kwa iliyokuwa Sheria ya Sukari kupitia kutekelezwa kwa Sheria ya Mimea mnamo mwaka 2013.
Utiaji saini wa Mswada wa Sukari 2022 unarejesha majukumu ya Bodi ya Sukari nchini ambayo kwa sasa yanatekelezwa na Kurugenzi ya Mamlaka ya Kilimo na Chakula.
Mswada huo utaiwezesha Bodi ya Sukari nchini, miongoni mwa mambo mengine, kudhibiti, kuendeleza na kukuza sekta ya sukari na pia kuratibu shughuli za watu binafsi na mashirika ndani ya sekta hiyo.
Aidha, utaiwezesha bodi hiyo kuagiza na kuuza sukari inayozalishwa humu nchini nje ya nchi, kuwashauri wakulima na kudhibiti bei za sukari sawia na kutoa leseni kwa kampuni za kusaga miwa.