Rais William Ruto Leo Jumanne, ametia saini kuwa sheria mswada wa marekebisho ya tume ya uchaguzi nchini IEBC wa mwaka 2024.
Hafla hiyo iliandaliwa katika jumba la mikutano ya kimataifa KICC, na kuhudhuriwa na viongozi wa kisiasa kutoka muungano wa Kenya Kwanza na Azimio la Umoja One Kenya.
Mswada huo ulipitishwa na bunge kufuatia mapendekezo ya ripoti ya kamati ya kitaifa ya maridhiano (NADCO).
Sheria hiyo mpya inatoa nafasi ya kubuniwa kwa tume ya uchaguzi nchini IEBC, pamoja na kuteuliwa kwa makamishna wapya wa tume hiyo.
“Kutiwa saini kwa Mswada huu kuwa sheria, kunatoa fursa ya kubuniwa kwa jopo litakalowateua makamishna wapya wa IEBC,” alisema Rais Ruto.
Rais Ruto alisema utawala wake utaendelea kutekeleza mapendekezo yaliyomo katika ripoti ya NADCO, kwa kuhakikisha umoja wa taifa hili
“Kutiwa saini kwa Mswada huu ni hatua kubwa katika kutekeleza mapendekezo yaliyomo katika ripoti ya NADCO na ni ishara ya uwezo wa taifa hili wa kukabiliana na changamoto na maswala ambayo huenda yakasambaratisha utangamano wa taifa na usalama,” alisema Rais Ruto.
Waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na kiongozi wa upinzani Raila Odiga, kinara wa wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa wengi bungeni Kimani Ichung’wa na kiongozi wa wachache Opiyi Wandayi miongoni mwa wengine.