Rais William Ruto ametetea uamuzi wake wa kushirikiana na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga, akisema hakuna kilichoharibika na ni wakati wa kuungana kuhudumia wakenya.
Ruto ambaye anaendeleza ziara ya eneo la Nyanza, aliyasema hayo huko Oyugis kaunti ya Homa Bay wakati alizindua mradi wa maji akielezea kwamba hatua hiyo inalenga kuunganisha wakenya.
Huku akihimiza kukomeshwa kwa siasa kuhusu suala hilo, Rais alikiri kwamba wakati mmoja alikuwa msaidizi wa Raila na sasa ni wakati mwafaka wa kurudisha mkono kwa kuunga mkono azma yake ya kuwania uenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika AUC.
Kiongozi wa nchi aliongeza pia kwamba Odinga alimsaidia kubuni serikali jumuishi ambayo inahusisha viongozi wa upinzani baada ya maandamano ya siku kadhaa.
Alikanusha madai kwamba hatua ya kuhusisha upinzani serikalini ilidhamiriwa kuua upinzani humu nchini na kufafanua kwamba yeye na Odinga walikubaliana kubuni serikali jumuishi kwa kuweka mawaziri kutoka upinzani.
Kulingana naye, Odinga anajali maslahi ya bara zima la Afrika na anastahili kuongoza bara hili kupitia uenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika.
Kuhusu maendeleo, Rais aliahidi kwamba atahakikisha uwepo wa masoko ya kisasa,barabara bora, maji na umeme katika sehemu mbali mbali nchiniili kuinua maisha ya wakenya.
Serikali yake alisema itaafikia mpango wa huduma bora za afya kwa wote kupitia kwa bima ya afya ya jamii SHIF.