Rais Ruto atetea mpango wa kuboresha barabara nchini

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amesema kwamba uamuzi wa kuwekeza katika uboreshaji wa barabara humu nchini utainua hadhi ya nchi hii na kuchochea biashara.

Akizungumza huko Nakuru jana Jumamosi alikozindua ujenzi wa barabara ya Kiambiriria-Kuresoi-Chepsir, kiongozi wa nchi alisema kila sehemu ya nchi hii itafikiwa katika mpango huo wa barabara ambao pia utachochea ukuaji wa uchumi na kutoa nafasi za ajira.

Kulingana naye, barabara hiyo ya kilomita 40 inayopitia eneo la ukulima la Kuresoi Kaskazini itarahisisha ufikiaji wa raslimali, fursa na huduma.

“Huu ndio wakati wa kunyoosha mambo, ni fursa yetu kubadilisha Kenya,” alisema Ruto ambaye kwa muda wa wiki moja iliyopita amezuru kaunti 4 kuzindua na kuzuru miradi ya barabara.

Waziri wa Uchukuzi na Barabara Kipchumba Murkomen kwa upande wake alisema kwamba hilo ni dhihirisho kwamba barabara ni muhimu kwa kuafikia fursa mbalimbali.

Jumatano iliyopita katika kaunti ya Laikipia, Rais Ruto alizindua uboreshaji wa barabara ya Ngobit-Withare-Limuria-Ngobit Girls na ile ya shule ya msingi ya Kihara.

Alhamisi alikuwa katika kaunti ya Nyandarua kuzindua mradi wa kuweka lami barabara ya kilomita 44 ya Boiman – Kwa Mumbi huko Ol Joro Orok.

Miradi mingine inayoendelea ni barabara ya kilomita 55 ya Captain Ndemi – Ndunyu Njeru, ile ya kilomita 41 ya Engineer – Gathera, ile ya kilomita 45 ya Maili Kumi – Shameta, ile ya kilomita 55 ya Shamata – Uruku, ile ya kilomita 23 ya Gilgil – Machinery na nyingine ya kilomita 28 ya Tumaini -Kabazi.

Barabara ambazo zimepangiwa kukarabatiwa ni pamoja na ile ya kilomita 14 ya Nyahururu – Boiman, ile ya kilomita 14 ya Maili Nne – Maili Kumi na ile ya kilomita 8 ya Kirasha – Sulmac.

Rais alisema kaunti ya Nakuru ina jumla ya kilomita 450 za barabara zinazoshughulikiwa na mamlaka ya KeRRA na kilomita 300 tayari zimekamilika.

Alitaja mpango huo kuwa mwanzo tu kwani Kenya nzima itashuhudia uboreshaji wa barabara.

Share This Article