Rais William Ruto amesema kuwa kurejeshwa kwa amani katika eneo la Bonde la Ufa ni hatua kubwa katika kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwenye eneo hilo ambalo hukumbwa na visa vya ujambazi mara kwa mara.
Rais alizipongeza jamii za eneo hilo na waliotekeleza jukumu katika kuhakikisha kwamba usalama umerejeshwa katika eneo hilo linalounganisha kaunti tatu za Elgeiyo Marakwet, Pokot magharibi na Baringo.
Akizungumza alipoongoza maombi ya madhehebu mbalimbali huko Tot, kaunti ya Elgeyo Marakwet, Rais aliwapongeza maafisa wa usalama kwa kujitolea kukomesha ujambazi katika eneo hilo.
Rais pia alisema kuwa serikali inaazimia kushughulikia changamoto mbalimbali zinazokumba taifa hili huku akitoa wito wa uvumilivu miongoni mwa wananchi.
Alisema kuwa serikali imechukua hatua zitakazohakikisha mabadiliko ya kiuchumi humu nchini.
Wakati huo huo Rais William Ruto alisema taifa hili limejinasua kutoka kwa utawala wa siasa za ukabila na migawanyiko uliotatiza maendeleo kwa miaka mingi.
Rais alisema kampeni za mapema kabla ya uchaguzi mkuu ujao sasa zimezikwa katika kaburi la sahau, huku akiwataka viongozi kushughulikia masuala yanayohusu wananchi.
Ruto alisema nchi imeanza kuvuna matunda ya uongozi ulioungana kupitia kubuniwa kwa serikali pana.
Mbali na udhabiti wa kiuchumi, kiongozi wa taifa alisema nchi hii inakaribia kuafikia ajenda ya kuhakikisha uwepo wa chakula cha kutosha kutokana na mikakati ya serikali ambayo imeboresha uzalishaji wa kilimo.