Rais Ruto asisitiza haja ya kutumia talanta kuchuma riziki

PCS
By
PCS
5 Min Read
Rais William Ruto amesema serikali inawekeza katika uchumaji mapato kupitia kwa talanta ili kuimarisha ujasiriamali, uvumbuzi na ukuaji wa uchumi.
Rais alisema serikali iko makini katika ubadilishaji wa talanta kuwa njia ya mapato, kubuni kizazi chenye uwezo na kinachojitegemea.
 Alitoa mfano wa Talanta Hela ambayo inahamasisha vijana kutekeleza malengo yao ya kisanii na michezo.
 “Mpango wa Talanta Hela ni programu halisi ya kutoka Chini kwenda juu; inayolenga kuhakikisha uwezeshaji, uundaji wa fursa na mabadiliko ya michezo, mambo ya vijana na sanaa,” alisema.
 Rais aliyasema hayo wakati wa ufunguzi rasmi wa Jumba la Talanta Plaza jijini Nairobi akiwa na Waziri wa Michezo Ababu Namwamba.
 Jengo hilo litakuwa makazi mapya ya Wizara ya Mambo ya Vijana, Sanaa na Michezo.
 “Mradi huu unaonyesha dhamira yetu kwa michezo, vijana na sanaa na sasa ni kitovu cha Mpango wa Talanta Hela, programu yetu kuu ya kuchuma pato kupitia vipaji katika nchi yetu,” alisema.
 Rais Ruto alisema serikali imejitolea kutoa miundombinu inayohitajika ili kuendeleza maendeleo ya michezo nchini.
 Alisema serikali inaboresha Uwanja wa Michezo wa Kimataifa wa Moi, Kasarani,  Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo na Uwanja wa Kipchoge Keino, mjini Eldoret.
 “Harakati hizi zitaongeza azima yetu ya kuwa wenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 pamoja na Uganda na Tanzania.”
 Rais Ruto alitangaza leo kuzinduliwa kwa Mashindano ya Uvumbuzi ya Rais, yanayolenga kukuza uvumbuzi na kusaidia vyanzo vya biashara.
 Alisema mpango huu unatarajiwa kuanza mwezi huu na utafikia kilele chake wakati wa Wiki ya Ubunifu ya Jumuiya ya Madola, ambapo ubunifu na vyanzo vya biashara bora vitatambuliwa.
 Alitoa wito kwa Hazina za Usawazishaji: Hazina ya Hasla, Hazina ya Maendeleo ya Biashara ya Vijana (YEDF), Hazina ya Biashara ya Wanawake (WEF), Hazina ya Uwezo na Hazina ya Serikali ya Kitaifa ya Usawazishaji (NGAAF) kubuni vifaa maalum vinavyolenga vijana katika nafasi za uchumi samawati, kijani na uchumi unaozingatia ubunifu wa akili almaarufu uchumi rangi ya chungwa.
 “Hii itasaidia katika kupunguza changamoto kuu zinazowakabili vijana nchini ikiwa ni pamoja na kiwango kikubwa cha uzembe, ukosefu wa ajira na ajira duni, mimba za utotoni na zisizotarajiwa, uhalifu, ulevi na matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa mambo mengine,” alisema.
 Waziri Namwamba aliipongeza timu ya riadha iliyowakilisha Kenya katika Mashindano ya Riadha ya Dunia mjini Budapest.
 Alisema serikali imeboresha zawadi ya fedha kwa wanariadha wanaoshinda medali wanapowakilisha nchi hii.
 “Pia tumelipa madeni yote yaliyosalia kwa wanariadha wetu kwa zaidi ya miaka 10,” alisema.
 Hapo awali, Rais Ruto alihudhuria Kongamano la Tabia Nchi la Vijana barani Afrika la 2023 katika Ukumbi wa Jumba la Mikutano ya Kimataifa la Kenyatta (KICC),  Nairobi kabla ya kufanyika kwa Kongamano la Afrika Kuhusu Tabia Nchi juma lijalo.
 Rais aliwataka vijana wa Kiafrika kuchukua jukumu kubwa katika hatua dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.
 Alisema vijana ndio wadau wakubwa wa mabadiliko ya tabia nchi akisema wao ndio walinzi wa siku zijazo.
 Alibainisha kuwa kuwaweka kando vijana itakuwa ni zoezi lisilo na maana.
 “Nawaomba vijana wa bara letu chukueni hatua, tuanzishe mabadiliko haya kwa pamoja,” alisema.
 Rais alisema kuwa Afrika inachukua nafasi ya uongozi katika hatua ya mabadiliko ya tabia nchi kwa kuhama kutoka kuwa mwathirika hadi mtoa suluhisho.
 “Tutabadilisha mtazamo wetu. Tutakuwa na mapendekezo, mawazo na mali na kutafuta njia yetu kuelekea kwenye meza,” alisema.
 Rais Ruto alitoa wito kwa mataifa ya Afrika kutumia nafasi inayotokana na hatua za tabia nchi ili kutengeneza fursa kwa vijana.
 Alibainisha kuwa wingi wa rasilimali za Afrika katika nishati mbadala unalipa bara nafasi ya kufaidika kutokana na hatua za tabia nchi.
 Alifafanua kuwa rasilimali hizi za nishati mbadala zitabuni fursa za kutengeneza ajira, uwekezaji na ubunifu.
 “Afrika ina uwezo wa kupanua uchumi na ustawi wake huku ikiepuka kuzidisha hali mbaya ya mabadiliko ya tabi anchi na kutoa suluhisho zinazozingatia umahiri dhidi ya tabianchi,” aliongeza Ruto.
PCS
+ posts
Share This Article