Rais Ruto asifia nishati safi, aitaja kuwa suluhu kwa mabadiliko ya tabia nchi

Martin Mwanje
2 Min Read

Taasisi za umma zimetakiwa kuanza kutumia nishati safi na endelevu.

Rais William Ruto amesema hatua hiyo itaharakisha utunzaji wa mazingira.

Amesema upatikanaji wa upishi safi ni sera yenye kipaumbele na ni muhimu kwa Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi ya Kuanzia Chini kuelekea Juu.

Alisema mkakati wa nishati anuwai umebuniwa ili kuongoza mchakato wa kuelekea upatikanaji wa nishati ya kisasa ya upishi duniani.

Rais Ruto aliyasema hayo leo Jumanne katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la KICC, Nairobi wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Nishati la Afrika.

Alisema kiini cha maono ya Kenya ni maendeleo ya nishati endelevu.

“Uwekezaji katika nishati mbadala sio tu chaguo la kuwajibika lakini pia njia ya kuelekea kwa Afrika iliyoendelea zaidi na yenye usawa,” alisema Rais Ruto.

Alisema hatua ya kuacha kutumia fueli kisukuku itachangia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Alisikitika kwamba licha ya Afrika kuwa mchangiaji mdogo wa mabadiliko ya tabia nchi, inasheheni mzigo mkubwa wa athari zake.

Kutokana na hili, Ruto alisema kuna haja kwa Afrika kuongeza utoaji miito ya kutaka juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kuchukuliwa.

Maendeleo ya nishati endelevu, alisema, yanahitaji kipimo toshelezi ili kuhakikisha upatikanaji wa nishati kwa bei nafuu duniani.

“Hii inahitaji kuwepo kwa sera jumuishi za nishati, mikakati bunifu ya ufadhili na kutekelezwa kwa sera lengwa ili kuwafikia wale wenye mahitaji zaidi,” alielezea.

Mawaziri Davies Chirchir wa Nishati, Peninah Malonza wa Utalii, Rebecca Miano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Moses Kuria wa Biashara ni miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *