Rais William Ruto amesifia mazungumzo ya maridhiano yanayoendelea ya pande mbili kati ya serikali na upinzani.
Mazungumzo hayo yamekuwa yakiongozwa na kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa wengi katika bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah.
Ukumbi wa Bomas umekuwa kitovu cha mazungumzo hayo yanayolenga kusuluhisha masuala nyeti ambayo kwa muda mrefu yamekuwa chanzo cha mikwaruzano ya mara kwa mara kati ya serikali na upinzani.
“Mazungumzo ya pande mbili yanayoendelea yamewawezesha viongozi wetu kuafikiana kuhusiana na masuala mengi ambayo utatuzi wake utasaidia kuharakisha mabadiliko yetu, kuboresha demokrasia na kukuza umoja wa kitaifa,” amesema Rais Ruto wakati akilihutubia taifa katika majengo ya bunge.
“Napongeza ujasiri na uzalendo wa viongozi wenzangu ambao wamekumbatia mazungumzo ya kitaifa na kutia moyo kila mmoja wetu kuendelea kuunga mkono kazi kubwa ya kuwaleta Wakenya pamoja.”
Rais alisisitiza kuwa siasa zinazoongozwa na sera ni muhimu kwa ustawi wa demokrasia na ni njia bora ya kuhakikisha mabadiliko endelevu nchini.
Kauli zake zikiwadia wakati ambapo Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo imetangaza kukamilika kwa mamlaka yake baada ya mazungumzo hayo kuendelea kwa kipindi cha siku 73 zilizopita.
Mwenyekiti mwenza wa kamati hiyo Kalonzo Musyoka anasema timu ya kiufundi inatarajiwa kukutana na kutayarisha ripoti ya mwisho itakayowasilishwa kwa Rais ikiwa na mapendekezo yanayopaswa kutekelezwa kwa manufaa ya taifa.