Kiongozi wa taifa Rais William Ruto ameshabikia uongozi wa wanawake humu nchini akisema una nafasi kubwa.
Akihutubia taifa katika uwanja wa michezo wa Kwale alipoongoza sherehe za siku ya Mashujaa, Rais alimtambua Gavana wa kaunti ya Kwale Fatuma Achani.
“Kama kungekuwa na tashwishi yoyote, kwamba mama muisilamu anaweza kuwa kiongozi na awe Gavana, sasa hiyo tashwishi imeondoka kwa sababu Fatuma Achani ni gavana wetu wa hapa Kwale.” alisema kiongozi wa nchi.
Rais aliendelea kusema kwamba sasa inaweza kuthibitika kwamba uongozi wa wanawake una nafasi nzuri na thabiti katika nchi ya Kenya.
Ruto aliridhishwa pia na jambo alilolitaja kuwa la kihistoria pale ambapo mwanajeshi wa kike Luteni Kanali Faith Mwangandi aliongoza gwaride ya heshima.
“Kudhihirisha tena kwamba kina mama wanaweza kufanya kazi zote.” Alisema Rais Ruto akimwashiria Luteni Kanali Faith Mwangandi huku akiutaka umati umpigie makofi.
Kwenye orodha yake ya mashujaa wa awali vile vile, Rais alimtaja mama Mekatilili wa Menza ambaye alisema hakutafuta uhuru wa kijiji chake pekee.
“Badala yake alikataa mifumo na taasisi za unyanyasaji na udhalimu akifahamu kwamba hivyo vikishindwa basi taifa zima litakuwa huru.” alisema rais William ruto.