Ruto asema yuko tayari kujadiliana na Jaji Mkuu Koome

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amesema kwamba yuko tayari kujadiliana na maafisa wa idara ya mahakama wakiongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome ili kutatua suala la ufisadi.

Rais alisema kutumia mkakati wa ushirikiano kati ya asasi tatu kuu za serikali ambazo ni afisi ya Rais, bunge na mahakama kutaimarisha vita dhidi ya ufisadi serikalini.

Kiongozi wa nchi alikuwa akizungumza katika kaunti ya Nandi wakati wa kuzindua taasisi ya mafunzo kwa walimu ya Tinderet ambapo alisema ufisadi unachelewesha utekelezaji wa miradi ya serikali.

Ruto alisisitiza kujitolea kwa serikali kulinda uhuru wa idara ya mahakama lakini akaongeza kwamba serikali itakabiliana vilivyo na ufisadi katika idara hiyo na kurejesha uamunifu wake.

Alisikitika kwamba watu wachache ambao hawataki kuona mabadiliko nchini wanatumia mahakama kukwamisha ajenda ya maendeleo ya serikali.

Nia ya watu hao ya kuhujumu maendeleo alisema ndiyo imemchochea kudhihirisha uongozi kwa kuandaa mkutano na uongozi wa idara ya mahakama.

Rais Ruto anasema Kenya imesalia nyuma kimaendeleo kufuatia uongozi mbaya na ufisadi na kwamba wakati umewadia wa kutekeleza maamuzi muhimu ambayo yataendeleza nchi.

Alikuwa ameandamana na naibu Rais Rigathi Gachagua, waziri Alice Wahome, Gavana wa Nandi Stephen Sang na kiongozi wa wengi bungeni Kimani Ichung’wah kati ya wengine wengi.

Ichungw’ah kwa upande wake alisema bunge liko tayari kuhusika kwenye majadiliano ya kukabiliana na ufisadi akimtaka jaji mkuu kuwahakikishia kwamba mahakama hazitatumika kulinda wafisadi.

Naibu Rais Gachagua alisema uchumi umeonyesha dalili ya mwelekeo mzuri huku akiomba wakenya kuunga Rais Ruto mkono ili afanikishe ajenda ya maendeleo.

Kando na uzinduzi wa taasisi hiyo Rais alianzisha ujenzi wa nyumba za gharama nafuu huko Emgwen , akazindua kiwanda cha kutayarisha nyama ya ndege kama kuku huko Kapsabet na akazindua chuo cha mafunzo ya kiufundi cha kitaifa cha Kaiboi.

Katika taasisi ya Kaiboi kiongozi wa nchi alizindua maabara ya teknolojia ya Jitume na kuweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa kituo cha teknolojia.

Alizuru pia kiwanda cha maziwa cha kaunti ya Nandi huko Kabiyet ambacho ujenzi wake umekamilikakwa kiwango cha asilimia 95.

 

Share This Article