Rais Ruto asema siasa za ukabila zimepitwa na wakati

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amesema kwamba siasa za ukabila zimepitwa na wakati na kwamba serikali sasa inaangazia uongozi wa maono wa kubadilisha maisha ya wakenya.

“Hakuna tena nafasi ya siasa za ukabila zinazotajirisha wachache na kuacha wengi wakitaabika,” alisema kiongozi wa nchi alipokuwa mwenyeji wa viongozi wa mashinani kutoka kaunti ya Murang’a.

Katika kikao hicho, Rais aliorodhesha mipango kadhaa ya maendeleo inayolenga kaunti ya Murang’a akitaja mradi wa nyumba za gharama nafuu wa nyumba 10, 300 za thamani ya shilingi bilioni 23.

Rais alisema pia kwamba serikali imetenga shilingi bilioni 3.5 za kuboresha barabara, bilioni 2.3 za ujenzi wa masoko ya kisasa 23 na bilioni 3 kwa ujenzi wa nyumba za makazi ya wanafunzi.

“Ili kuharakisha ujasiriamali na ukuaji jumuishi, familia elfu 10 zitaunganishiwa umeme kufikia Disemba kupitia mpango wetu wa milioni 850 wa umeme.” Alisema Rais.

Ruto alisema pia kwamba serikali imejitolea kujenga viwanja viwili vya michezo vya kisasa katika kaunti hiyo kwa gharama ya shilingi bilioni 1.5 kando na kuweka maji katika maeneo ya Kangema, Mathioya, Kiharu na Kandara chini ya mradi wa bilioni 2.4 wa maji.

Kiongozi wa nchi amekuwa akikutana na viongozi wa maeneo mbali mbali katika ikulu ya Nairobi wa hivi punde zaidi wakiwa wa eneo la Gusii ambapo amepangiwa kuzuru.

Hivi leo Jumamosi anapangiwa kukutana na viongozi waliochaguliwa wa walimu nchini.

Website |  + posts
Share This Article