Rais William Ruto amesema kwamba mji wa Bomet ambao ni makao makuu ya kaunti ya Bomet utapanuliwa.
Alikuwa akizungumza wakati wa kuzindua shughuli ya kukarabati barabara ya links mjini Bomet ambapo aliongeza kwamba uboreshaji huo unalenga kutosheleza idadi inayozidi kuongezeka ya wakazi mjini humo.
Rais Ruto ambaye alikuwa ameandamana na naibu Rais Rigathi Gachagua, alizuru pia mradi unaoendelea wa nyumba za bei nafuu wa Bomet ambapo nyumba 220 zinajengwa.
Alitumia fursa hiyo kuwasihi wakazi wa Bomet kuunga mkono mpango wa serikali wa kiuchumi Bottom Up, kwa manufaa ya kila mmoja wao.
Mpango wa kuunganisha stima mashinani wa Chemomul huko Bomet Mashariki ulizinduliwa pia na Rais Ruto.
Alisema lengo ni kuunganisha kila boma na umeme huku mpango wa kawi safi isiyochafua mazingira pia ukizingatiwa.
Gavana wa Bomet Hillary Barchok alikuwa na Rais kwenye ziara hiyo pamoja na viongozi wengine wengi.