Rais Ruto asema amejitolea kumaliza aibu ya njaa

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amesema amejitolea kumaliza kabisa aibu ya njaa nchini ndiposa alianzisha mpango wa kusajili wakulima kwenye mpango wa mbolea ya bei nafuu ambao umesababisha ugavi wa magunia milioni 5.5 ya mbolea humu nchini.

Akizungumza bungeni alasiri ya leo wakati wa kutoa hotuba kuhusu hali ya nchi hii, Rais alisema gharama ya juu ya maisha inaathiri wakenya wote na hali hiyo inaweza kusuluhishwa kupitia sera na vitendo faafu.

“Mojawapo ya njia za kusuluhisha gharama ya juu ya maisha ni mkakati wa kupiga jeki uzalishaji wa chakula na mimea ya kuuza pamoja na kuimarisha sekta ya ufugaji.” alisema kiongozi wa nchi.

Alielezea kwamba gharama ya mbolea ilipunguzwa kutoka shilingi elfu 6,500 hadi 2,500, na hivyo kuongeza ardhi inayotumiwa kwa kilimo cha mahindi kwa ekari laki 2 zaidi. Hatua hiyo imeongeza mazao kwa magunia milioni 18.

“Kutokana na mipango hiyo, leo pakiti ya kilo mbili ya unga wa mahindi inauzwa kwa kati ya shilingi 145 na 175 kutoka bei ya awali ya shilingi 250.” alisema Rais akiongeza kwamba sasa mkebe wa kilo mbili za mahindi makavu sasa unauzwa kwa shilingi 60 hadi 75.

Kiongozi wanchi alifika bungeni kuhutubia kikao cha pamoja cha bunge la taifa na bunge la seneti kuhusu hali ya nchi inavyohitajika kisheria.

Website |  + posts
Share This Article